JAMBO FORUMS WATENDEWE HAKI
Na Fungo, Augustus[1].
Hivi karibuni kumekuwapo taarifa juu ya kukamatwa vijana wawili wakihusishwa na mtandao maarufu wa tovuti uitwao jambo forums. Mtandao ambao ulikuwa ukipatikana kwa anuani hii www.jamboforums.com popote duniani. Vijana hawa walishikiliwa na polisi kwa zaidi ya saa 24 wakihojiwa na baadaye kuachiliwa kwa dhamana. Baadaye ilifuatiwa taarifa ya mwanachama mwandamizi wa jambo forums katika BBC akieleza kusikitishwa kwake na kukamatwa kwa wanachama hao,ambapo maelezo yake yalijibiwa kwa maelezo toka kwa msemaji wa jeshi la polisi kuwa mtandao huu unatoa habari za uongo,ni wa kichochezi na unahusishwa na ugaidi. Mbali ya kuzungumzia mambo ya cyber crimes, mkuu huyo toka polisi aliuhusisha moja kwa moja mtandao huu na ugaidi ikiwa ni pamoja na kusema kuna watu wamelalamikia mtandao huu kuwa unawachafua majina yao. Mwandishi wetu katika makala haya anajaribu kuchambua kauli hizo kwa kulinganisha na kile kinachofanyika jambo forum na sheria zetu zilizopo.
Labda tuanze kuangalia jambo forum ni nini na inafanya nini.
Kwa watu wachache ambao wamepata kuuona mtandao huu kwenye internet(kwani internet sio siri)mimi nikiwa mmojawapo, watakubaliana na mimi kuwa ni vigumu kuamini kuwa mtandao huu ni wa kigaidi kutokana na mambo yaliyomo mule labda kama polisi wana vigezo vingine na maana nyingine ya ugaidi tofauti na ile iliyopo kwenye sheria ya kuzuia ugaidi ya mwaka 2002 yaani Prevention of Terrorism Act. Jambo forum ni mtandao ambao unaitwa jukwaa la majadiliano ambapo watu wa kada mbalimbali huruhusiwa kutoa maoni yao kuhusu mada yoyote iliyowekwa humo. Aidha watu huruhusiwa kuuliza maswali na kujibizana ikiwa hata kukanushana wenyewe kwa wenyewe.Mtandao huu hautofautiani kabisa na unapowakuta watu pale Manzese, kariakoo,au Nkurumah chuo kikuu cha Dar-es-salaam wakijadiliana jambo, hivyo daima kutakuwa na pande mbili zinazopingana,wale wanaokubali hoja na wale wanaopinga hoja. Haya ndiyo yanayofanyika jambo forum.Tena mtu akiandika kitu ambacho hana uhakika nacho wachangiaji watamshambulia sana hadi kupelekea mada hiyo kufungwa. Suala la kujiuliza hapa je hizo mada zinatoka wapi? Mada hizi,hutokana na mambo ya kila siku yanyoibuka na kuendelea Tanzania na duniani pote na hasa yale yaliyoandikwa kwenye magazeti ya kila siku.Mada nyingine ni kweli huwa za kutungwa hasa zile zilizo mfano wa maswali. Hapa nitatoa mfano kidogo. Hivi karibuni nchini Tanzania kulikuwa na matukio ya kufukuzwa kwa Gavana wa benki kuu,ripoti ya richmondi na ujio wa Rais Bush wa marekani,mada zilizotawala mtandao huu toka wakati wa sakata la BOT zilikuwa,je,Balali ashtakiwe?,Je,Ziara ya Bush nchini Tanzania haina faida yoyote kama baadhi ya watu wanavyosema?,Je,Hosea atakwepa dhambi ya kujiuzulu kwa mujibu wa ripoti ya mwakyembe na suala la hotuba ya Rais Kikwete na Bush wakiwa ikulu darn a jinsi vyombo vya magharibi vilivyoiandika.Hivyo kwa ufupi jambo forums ni jukwaa la majadiliano.
Tofauti na lilivyo gazeti ambapo habari hutolea na mhariri na msomaji hana nafasi ya kuidadisi habari hiyo au kuuliza maswali au kuchangia jambo;Jambo forum msomaji wa mada(tena sio habari) mada hupata nafasi ya kuchangia, kuuliza maswali, hata kutofautiana kabisa na mwandishi kwa kuja na hoja tofauti yenye ushahidi na vigezo mahiri. Aidha pamoja na mada kama hizi zinazohusu siasa kuna sehemu ya mtandao huu ambayo hujadili habari kuhusu Afrika mashariki, uchumi, elimu, sheria, maswali, afya, burudani na michezo, dini, pamoja na lugha. Katika hizi mada nyingine utakutana na majadiliano kuhusu sayansi ya teknolojia, utakutana na masuala ya uchaguzi wa marekani,utakutana na maneno mbalimbali ya Kiswahili jnsi yanavyotumika na kukosolewa na vilevile masuala ya dini. Katika kuchangia mada hizi wachangiaji ambao idadi yao ni zaidi ya elfu nne wenye elimu na nyadhifa mbalimbali serikalini na nje ya serikali,na waliotawanyika popote duniani na ambao ni watanzania,huchangia mada hizi kutokana na uelewa wao wa mada hizo na wasipoelewa huomba nafasi ya kuuliza toka kwa wale wanaoelewa na hata wakipewa majibu basi wao huyachallenji.Hata baadhi ya waheshimiwa muhimu wa hapa Tanzania hutoa mada kwenye mtandao huu. Na kizuri zaidi katika mtandao huu,mada ya yoyote inayojadiliwa mara nyingi huwa haina hitimisho zaidi ya kukosa wachangiaji na matokea yake kufungwa,katu hata siku moja watu hawatoki na azimio Fulani au kupanga namna ya kutekeleza majadiliano haya.Na kila siku huibuka mijadala mipya na mingine kufa.Sasa sijui suala la ugaidi linatoka wapi? Je,mtu anayechangia misamiati ya Kiswahili ili kukuza lugha ugaidi wake unatoka wapi? Mtu anayechangia mada kuhusu ugonjwa wa malaria, teknolojia, mauaji ya Kenya na kuomba watu waishi kwa amani anatoa habari zipi za uongo au ugaidi?
Ni ukweli usiofichika kuwa katika jukwaa la siasa, jambo forum au jf kama wao wanavyoiita,imekuwa ikiibua mambo mazito katika jamii yakiwemo masuala ya buzwagi, richmondi, EPA,TICTS na mengineyo mengi ambayo yamepelekea habari nyingi kwenye vyombo vya habari hadi bungeni na hata kuundwa kamti ya mwakyembe ambayo sote matokeo yake tumeyaona.Habari hizi wakati mwingine zimekuwa zikigusa idara muhimu za serikali, maafisa wake na hata chama tawala kama vile This day, kulikoni na mwanahalisi zinavyofanya. Aidha katika siku za karibuni jambo forum imekuwa mstari wa mbele kusisitiza kufanyiwa kazi kwa ripoti ya mwakyembe ikiwa ni pamoja na kuchambua uwajibikaji wa mtu mmoja mmoja kwenye ile ripoti,jambo ambalo sidhani kama ni kosa.Kwani hata hukumu iliyotolewa na mahakama watu wanahaki ya kuichambua.Inawezekana kabisa,ni kwa sababu hizi labda ndio maana jf inatajwa kama mtandao wa kigaidi kutokana na kufukua maovu mengi katika jamii na kuyaweka hadharani watu wachangie na mwishowe wajibu ni wao kuchukua ama kutochukua hatua.
Matumizi ya majina
Katika kujadili mada mbalimbali kwenye tovuti hiyo watu hutumia majina mbalimbali, bandia na yasiyo bandia,kwa maana ya kwamba baadhi hutumia majina yao halisi, anuani za barua pepe, na wengine hutumia majina ya kubuni. Hii haina maana kwamba wanaotumia majina bandia ni wahalifu. Kwani wakati wa kutoa maoni hakuna sheria yoyote inayomtaka mtu ataje jina lake kwanza ndipo atoe maoni. Hata wao Polisi mara nyingi wamekuwa wakituomba wananchi kuwapa habari kuhusu vitendo vya uhalifu bila kutaja majina yetu au hata kama tukitaja kwa maelezo kwamba watatuhifadhi. Sasa je,kuna ubaya wowote wa mtu kutotaja jina lake? Nchi zilizoendelea kama Uingereza,ipo sheria kuhusu uhifadhi wa habari za mtu(Data protection Act) ambapo kwa mujibu wa sheria hii mtu anayo haki ya kutotaja jina lake. Aidha majina mengi yanayotumika kwenye forum ni ya kisanii zaidi kuliko kuwa bandia mathalani mtu anajiita mwanakijiji, maskini jeuri, mtanzani halisi n.k.hayana uhusiano wowote na jinai. Hivyo kuufungia mtandao huo kwa mada moja tu ya kisiasa bila kuangalia content zake nyingine ni kukiuka uhuru wa watu kutoa maoni kwani si kweli kuwa habari zilizo katika mtandao huo zote ni za uongo. Hivi watu wanapojadiliana, nani anamdanganya nani?Isitoshe wachangiaji mada katika mtandao ule wana elimu zinazolala kati ya darasa la saba na phd,na asilimia 60 ya wachangiaji wanaonekana kuwa na elimu kati ya form six na chuo kikuu. Aidha wachangiaji wa jf wana itikadi tofauti wapo wa chama tawala na wa vyama vya upinzani, webye dini na wasio na dini,wanaoguswa na habari hizo na wasioguswa moja kwa moja.
Jaji mmoja wa mahakama kuu ya Tanzania katika kesi ya TAKRIMA[2] aliwahi kusema (wakati akijibu hoja ya serikali kuwa sheria ya takrima ililetwa ili kuondoa matumizi mabaya ya haki ya kushtaki katika mahakama kuhusu makosa ya uchaguzi)kwamba,ukweli kwamba haki au uhuru Fulani unatumika vibaya si sababu ya kuufuta au kuizui haki hiyo,kinachotakiwa ni kutafuta mbinu za kuboresha kwa kuondoa matumizi mabaya. Sote tunafahamu kwamba kila mtu ana haki ya kutoa maoni yake kwa mujibu wa ibara ya 18 ya katiba yetu,aidha sheri haisemi ni maoni gani,au yatoleweje.Japokuwa kimsingi hakuna haki bila wajibu,au hakuna haki isiyo na mipaka,bado mipaka hiyo isitumike vibaya. Twafahamu kuwa haki yako inapoishi ndipo ya mwingine inapoanza. Hivyo mtu yeyote angtegemea kwamba,mtu au watu waliokashfiwa kwenye mtandao huo waende mahakamani kwani tayari hiyo ni defamation sio criminal case. Na suala kwamba mtandao huo umesababisha watu wapigane au ugomvi wa baba na mwana,halina msingi kwani ni habari ngapi zinazoandikwa magazetini na watu kuishia kushikana mashati huko mtaani?Je,tunadhani habari zote zinazoandikwa kwenye magazeti watu wanazifurahia?vikatuni je? Naam hii ya jeshi la polisi kukemea mitandao kama jambo forum inanikumbusha miaka ya tisini ambapo aliyekuwa waziri wa mambo ya ndani wa wakati huo Ernest Nyanda alipiga marufuku vikatuni. Watu kama kina kipanya walipata shida sana wakati ule.Lakini je,vikatuni vimeondoka Tanzania? Tujiulize,hivi ni gaidi gani mjinga anayeweza kujadili mambo kwenye internet ambako hakuna usiri wowote? Kama ni hiyo cyber crime polisi wanayosema, sijui wanaielewaje? Nadhani vitivo vyetu vya sheria vinapaswa kuanza kufundisha somo la cyber crimes. Kwani kwa jinsi navyoelewa cyber crimes hazitokani na majadiliano.
Cyber crime[3] inahusu vitendo vya jinai vinavyohusu matumizi ya kompyuta na netiweki yaani kwa kiingereza “hacking” mfano kuiba website ya mtu na kubadilisha matumizi yake,kuharibu data,wizi wa kutumia internet,matangazo ya biashara feki,udanganyifu wenye lengo la kujipatia pesa au mali(fraud),wizi wa utambulisho wa mtu na kutumia visivyo(identity theft) na kutengeneza akaunti za credit card bandia.Pia inahusu picha za ngono za watoto,vitisho kwa kutumia barua pepe, maelezo ya matusi yanayohusu ngono na utupu na usambazaji wa habari chafu. Sasa je,katika hayo hapo juu,jf imefanya lipi?
Kama ni maelezo ya Uongo au habari za uzushi ziko tovuti nyingi kwenye ambazo zimekuwa zikionesha barai za ngono,na zisizo za kweli na pia yapo hata magazeti Tanzania tunayaita ya udaku ambayo habari zake nyingi zimekuwa za kutungwa ama ukweli wake unasuasua. Ikumbukwe kuwa Tanzania tofauti na nchi zilizoendelea hatuna sheria zinazotawala internet. Na hili ni tatizo kubwa ambalo mimi na wadau wengine tulidhani wakati umefika kwa polisi na wizara husika kufikiria kuwa na sheria hizi. Zaidi ya kanuni ya adhabu(pena code),sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai,(Criminal procedure Act)hatuna sheria ya msingi kabisa inayogusa cyber crime. Mbona mwaka Fulani hapa tovuti ya serikali iliibwa na bwana mmoja na ikatumika kuoneshea picha za ngono,Yule bwana tulishindwa kumfanya chochote? Nadhani umefika wakati Tanzania kuwa na sheria kama vile Data Protection Act, Fraud Act, Computer Misuse Act na Information and communications Act ambazo labda ndizo zitawawezesha polisi kudhibiti matumizi ya internet. Kutokuwa na sheria hizi polisi watajikuta wakilazimisha makosa kuingia katika sheria ambazo haziyataji makosa hayo. Na kesi zinazohusiana na internet si rahisi kama wao wanavyofikiri.Nje ya sheria hizi polisi watajikuta wanavunja sana haki za binadamu. Na ndio maana tunasema kwamba jambo forum watendewe haki,polisi waseme ukweli,je,sababu walizozitoa ni za kweli au kuna jambo jingine lililojificha?.
Mtakumbuka kuwa mwaka 2007 kulikuwa na habari kwenye internet kuhusu ubadhirifu wa pesa za BOT na wabadhirifu hao kutajwa.Pamoja na wananchi kutaka hatua zichukuliwe juu ya watu hao,na polisi kufanya uchunguzi.Polisi hao hao na baadhi ya wanasiasa walitoa majibu kuwa hawawezi kufanyia kazi habari za internet,kwani nyingi ni za uzushi na wala hawajui nani mwandishi.Tukasema sawa, lakini jeshi la polisi hilohilo leo limegeuka na kuanza kufanyia kazi habari za internet. Ndio kusemaje hapa,au kwakuwa zile za awali ziliwagusa baadhi ya watu ndani ya jeshi la polisi? Na hizi za sasa haziwagusi? Hebu tuwe consistent. Tuache watu watoe maoni.Tuache watu wajadiliane,hivi ukiwakuta watu wanajadiliana jambo Fulani pale kariakoo utawakamata eti kwa kuwa tu wanamjadili waziri mkuu aliyeondoka? Uhuru wa vyombo vya habari utainua taifa. Wenzetu katika nchi zilizoendelea mtu anaweza hata akasimama barabarani na bango kubwa ukasema “simtaki Gordon Brown kwa kuwa amefanya a,b,c.” Polisi hawatamfanya kitu maadamu haathiri haki za watu wengine. Wapo watakaokuunga mkono na pia wapo watakaomdharau tu. Ifike wakati tuache kufanya mambo kisiasa, tushughulike mamilioni ya EPA,TICTS,BUZWAGI n.k kuliko kushughulikia majadlianoya watu yasiyo na kichwa wala miguu.Mtu ambaye amekwazwa na jambo forums aende mahakamani,polisi wamsaidie tu kujua nani mmiliki wake ili aweze kumpelekea summons kwa urahisi.Sheria za madhara(torts) zipo zitumike.
Aidha, Ikumbukwe kuwa ni vigumu kudhibiti matumizi ya internet hasa bila kuwa na sheria pia ushirikiano wa wadau na nchi nyingine za afrika au duniani. Leo utawakamta hao vijana wawili kuwa ndio wanaohusika,lakini bila kujua hasa nani anamiliki hiyo server,utawafunga na kuwafanya lolote uwezalo,lakini kama server iko uingereza au marekani bado internet itaendelea kuwa hewani,na watu wataendelea kuandika na hapa ndio linakuja suala la jurisdiction. Je,unayo-jurisdiction ya kuzuia flow ya internet? Nadhani polisi walikurupuka,wajipange na waliangalie upya jambo hili na wakati mwingine kabla ya kuchukua hatua wawe wanaomba ushauri kwa wanazuoni wengine. Tunaliamini sana jeshi letu na tunajua kuna wasomi wengi lakini,kusoma hakuishi na mtu huwezi kuwa mtaalamu kwenye fani zote na ndio maana kuna mashauriano(consultation). Hili likifanyika tunadhani jeshi letu la polisi litaweza kufanya kazi vizuri zaidi kwa faida yetu sote.
Mwisho,natoa mwito kwa jeshi letu la polisi kujipanga na kufnya kazi kisayansi, kuwa na uchunguzi makini ili kutoathiri haki za watu. Na sio lazima kila wakati mtu akiripoti jambo kuhusu mtu Fulani umkamate hapohapo huyo mtu,upo uwezekano wa kufanya uchunguzi bila mtu huyo kujua halafu ndio unamkamata.Memetuambie mnachunguza suala hili,tunashukuru lakini hata kama hili suala linachunguzwa,basi lisiathiri uhuru wa watu na haki zao kikatiba, ili wananchi tujue habari za uongo katika mtandao huo ni zipi? Nani aliathirika nazo na hatimaye haki iweze kutendeka.Kwa upande mwingine mwito ni kwamba polisi waache kujumuisha mambo(generalisation) kwamba mtandao huu ni wa hivi na vile,kabla ya kuongea wafanye utafiti,kwani kauli wanazozitoa wkwa umma ni kauli nzito na zinawakilisha msimamo wa serikali.Hivyo ni vema zikatolewa baada ya kufanya utafiti wa kina na sio wa kuambiwa.Pia ni vema polisi nao wakaingia kwenye mtandao huo wakaona kinachofanyika na kwa sasa wawaruhusu wanaouendesha mtandao huo wauweke hewani ili wananchi wajue ukweli na waweze kuisaidia polisi katika uchunguzi wake.
[1] Mwandishi wa makala hii ni Mwanasheria binafsi na anayebobea katika masuala ya sheria za kimataifa za biashara, internet na jinai zake.Anapatikana kwa barua pepe augustoons@gmail.com
[2] Legal and Human Rights Centre and others v. AG [2005] HCT-DSM(Haijaripotiwa)
[3] http://www.naavi.org/pati/pati_cybercrimes_dec03.htm
Comments