NAMNA YA KUFUNGUA SHAURI LA MADAI YA MADHARA YA AJALI MAHAKAMANI


Namna ya kufungua shauri la madai kwa madhara ya ajali

Lusungu Hemed

WIKI iliyopita niliacha maswali kadhaa ambayo niliahidi kuyatanzua leo. Maswali haya ni: je, ni kitu gani kitaashiria kwamba sasa muathirika anaweza akachukua hatua ya kufungua shauri la madai? Je, kama muathirika ndiye aliyekufa ajalini, shauri hilo litafunguliwaje na nani atalifungua? Je, shauri linafunguliwa dhidi ya nani?
Leo nitajaribu kwa kiasi fulani kinachotosha kuyajibu maswali haya. Tuanze na swali la kwanza. Awali ya yote tulio wengi tunaweza kubaini kwa urahisi tu kama gari ilikuwa kwenye mwendo wa kasi mno au vipi.
Mara nyingi tumeshuhudia ajali zikitokea kutokana na mwendo wa kasi mno, au kutokana na magari kufukuzana. Hizi zote ni dalili za uzembe barabarani na ajali ikitokea, bila shaka mtu anaweza akachukua hatua ya kutaka ushauri wa kisheria ili afungue kesi ya madai.
Mara nyingi itokeapo ajali askari wa usalama barabarani hufungua mashitaka dhidi ya dereva aliyehusika. Ushahidi unaotolewa kwenye shauri la trafiki au kesi ya ajali ya barabarani, unaweza kutumiwa vile vile kujenga shauri la madai dhidi ya wale ambao uzembe wao ulisababisha ajali ya barabarani na hivyo kupelekea madhara kwa wahanga.
Pili, je, kama muathrika ndiye aliyepoteza maisha ni nani anapata haki ya kufungua kesi ya madai? Katika ajali kuna waathirika wa aina mbili.
Kwanza kuna yule ambaye atanusurika, kwa maana ya shauri la madai yeye mwenyewe, moja kwa moja.
Halafu kuna yule ambaye amepoteza maisha katika ajali. Kwa mtu kama huyu wale jamaa zake aliowaacha nyuma ndiyo wanakuwa waathirika. Sheria inawatambuia kama waathirika watu ambao walikuwa wnamtegemea marehemu katika kujkimu maisha yao.
Kwa mfano; endapo mzazi au ndugu mkubwa, mume au mke au mwandani, ndiye aliyefariki basi yule aliyekuwa akimtegemea au wale waliokuwa wakimtegemea wanakuwa ndiyo waathirika na kisheria wanaweza kufungua shauri la madai.
Hata hivyo, Sheria ya Ajali Sura ya 360 ya sheria za Tanzania inaweka utaratibu maalumu wa kufungua shauri pale ambapo jamaa ya marehemu aliyefariki katika ajali wanataka kufungua madai. Hawa wanapaswa kufungua shauri la madai kwa kumtumia mtu aliyeteuliwa kisheria kusimamia mirathi ya marehemu.
Vile vile, shauri hilo lazima lifuguliwe kwa niaba ya wale waliokuwa wakimtegemea. Ikumbukwe tu kwamba ipo Sheria ya Ukomo wa Kufungua Mashauri (The Law of Limitation Act, 1971). Sheria hii inaweka ukomo wa watu kufungua mashauri. Kwa upande wa mashauri yanayotokana na Sheria ya Madhara ukomo ni miaka 3. Yaani kama ajali imetokea mwezi wa kwanza mwaka 2007, basi ni sharti shauri la madi lifunguliwe ndani ya kipindi kisichozidi miaka mitatu toka ajali itokee.
Baada ya kujadili kiujumla hali hii ilivyo kuhusu Sheria ya Madhara, ni vema sasa tukaangalia ni anina gani ya madhara yanayomwezesha muathirika kufungua kesi ya kudai fidia.
Kwa ujumla sheria ya madhara inampa muathirika haki ya kudai fidia kwa ajili ya majeraha aliyopata mtu kutokana na ajali, vile vile haki ya kudai fidia kwa ajili ya mali yoyote aliyopotea wakati wa ajali.
Kimsingi, haki ya fidia imesimama katika dhana ya kwamba muathirika anatakiwa afidiwe kwa kiwango ambacho yaweza kusemekana kuwa amerejeshwa katika hali ile ile aliyokuwamo ya kwamba katika hali halisi si rahis mtu aliyeumia kurejeshwa katika hali ile ile aliyekuwemo kabla ya ajali kutokea. Kinachofanyika ni kwamba mahakama hujitahidi kutoa fidia ya kifedha kadri itakavyoruhusu ili kumpoza muathirika kwa madhara aliyopata kutokana na ajali.
Mtu anapopata madhara kutokana na uzembe wa mtu mwingine anakuwa na haki ya kudai aina mbili za fidia. Kuna ‘fidia ya jumla’ (general Damages), hii inaitwa fidia ya jumla kwa sababu makisio yake yanatokana na dhana kwamba ajali yoyote husababisha aina fulani ya msukosuko, aina fulani ya maumivu ya kimwili au ya kiakili na kadhalika.
Aina ya pili ni ‘fidia mahsusi’(specific damages). Hii huitwa mahususi kwa sababu haifanyiwi makisio ya jumla bali hutolewa kutokana na gharama halisi ya madhara yenyewe. Labda tutoe mifano ili wasomaji wangu muweze kunielewa zaidi. Mfano mzuri wa madhara ambayo hutolewa ‘fidia ya jumla’ ni maumiu.
Ni jambo lililo wazi kwamba mtu akikumbwa na ajali lazima atapata maumivu kwa kiwango fulani. Hivyo basi muathirika anaweza akadai fidia kwa ajili ya maumivu aliyuopata. Vile vile muathirika anaweza akadai fidia kwa ajili ya maumivu ya kiakili (kisaikolojia) aliyoyapata. Haya yote hutolewa ‘fidia’ au makisio ya jumla kwa sababu thamani yake halisisi haipimiki. Kiwango cha fidia ya jumla hukadiriwa na mahakama kwa kuzingatia mazingira yote ya ajali, ripoti za daktari na kadhalika.
‘Fidia mahsusi’ hutolewa kutokana na gharama halisi. Kwa mfano. kama mtu alilazwa hospitali ni rahisi hesabu na kupata gharama halisi kama vile za malazi hospitalini gharama za dawa na kadhalika. Vile vile kma katika ajali hiyo mtu atathibitisha kwamba alipoteza mali ya aina fulani, hiyo ni rahisi kupata gharama zake.
Baada ya kueleza kwa ujumla ni aina gani za fidia kuathirika kwa ajali anaweza kudai, wiki ijayo tutaendelea na mfululizo wa makala hii kwa kuangalia kwa undani kipengele kimoja kimoja kinchomwezesha muathirika kudai fidia.
Kwa majibu ya maswali haya tukutane wiki ijayo. Kwa maswali, maoni au kutaka ushauri, wasiliana na mhariri wa makala au na mwandishi kwa barua pepe hii
magondza@yahoo.com

Comments

Popular posts from this blog

PASSING OF PROPERTY IN THE GOODS

PASSING OF PROPERTY IN THE GOODS

SOURCES OF LAW