TAARIFA YA WAZIRI MKUU KUHUSU UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA BUNGE KATIKA MKATABA WA RICHMOND
TAARIFA YA WAZIRI MKUU, MHE. MIZENGO P. PINDA, (MB.), KUHUSU UTEKELEZAJI WA MAAZIMIO YA BUNGE YA MKATABA BAINA YA TANESCO NA RICHMOND DEVELOPMENT COMPANY LLC28 AGOSTI 2008 UTANGULIZI: 1. Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa kifungu cha 37(1) cha Kanuni za Kudumu za Bunge (Toleo la 2007), naomba kuwasilisha Taarifa ya Serikali kuhusu Utekelezaji wa Maazimio ya Bunge ya Mkataba baina ya TANESCO na Kampuni ya Richmond Development Company LLC. 2. Mheshimiwa Spika, Katika Mkutano wa Kumi wa Bunge tarehe 15 Februari 2008, Bunge lako Tukufu lilipitisha Maazimio 23 baada ya mjadala wa Taarifa ya Kamati Teule ya Bunge iliyoundwa mwezi Novemba 2007 ili kuchunguza mchakato wa Zabuni ulioipa ushindi Kampuni ya Richmond Development Company LLC wa kuzalisha umeme wa dharura Nchini mwaka 2006. Kwa kuzingatia uzito wa suala hili, wakati nilipotoa Hotuba yangu ya kuahirisha Mkutano wa Kumi wa Bunge nilieleza kuwa Serikali itaunda Timu ndogo ya Wataalam ili kuchambua kwa makini na kupendekeza namna ya kuteke...